Friday , 13th Jan , 2023

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Simon Maigwa, amesema wao wanachojua mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi alijinyonga kutokana na msongo wa mawazo, hivyo hayo masuala ya kwamba alimpa Iphone 14 mpenzi wake ni maneno tu na hayajathibitishwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Simon Maigwa

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 13, 2023, wakati akizungumza na East Africa TV & EA Radio Digital, na kusema wao bado wanaendelea na uchunguzi, na kuwa hawawezi kusikiliza maneno ya watu na kuachana na uchunguzi wao waliouanza.

"Mimi ninachojua kuna tukio la mwanafunzi kujinyonga uchunguzi bado tunaendelea, lakini kikubwa kifo chake kinatokana na msongo wa mawazo, yule ni mwanafunzi huwezi kujua je ni stress za masomo, hii kwamba alikuwa na mahusiano siwezi kukanusha au kukubali kwa sababu uchunguzi unatakiwa usibahatishe kutoa taarifa, hayo maneno yanasemwa na watu na sisi hatujayathibitisha (Kisa cha kumnunulia simu mpenzi wake)," amesema ACP Maigwa.

Mitandaoni kumekuwa na maneno yanayodaiwa kwamba mwanachuo huyo Gunze Luhangija mkazi wa mkoani Mwanza, alijinyonga baada ya kumnunulia mpenzi wake Iphone 14 na kisha kumkataa na ndipo kijana huyo alipoamua kujinyonga.