Friday , 3rd Feb , 2023

Marekani imetoa wito wa kukamatwa tena mara moja kwa mtu mmoja nchini  Sudan aliyepatikana na hatia ya mauaji ya mwanadiplomasia wa Marekani miaka 15 iliyopita. 

 

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia imemuita balozi wa Sudan mjini Washington kuhusiana na utata wa kuachiliwa huru kwa mshtakiwa Abdel Raouf Abu Zaid.

Zaid alikuwa akikabiliwa na adhabu ya kifo kufuatia mauaji ya mwanadiplomasia John Granville na dereva wake raia wa Sudan Abdel Rahman Abbas siku ya mwaka mpya mwaka 2008.

Marekani imetaja madai ya uwongo ya Sudan kwamba familia ya Bw Granville ilimsamehe muuaji huyo.Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imekanusha kuwa kuachiliwa huru ni sehemu ya makubaliano kati ya nchi hizo mbili.

Bwana Granville na mwenzake wa Sudan Bw Abbas wote walifanya kazi katika Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa nchini Sudan. Walipigwa risasi na kuuawa na watu wenye silaha walipokuwa wakitoka katika sherehe ya mwaka mpya mwaka 2008.