Mwanafunzi Laurence Mwangake
Inadaiwa sababu ya mwanafunzi huyo kuadhibiwa ni kutokana na walimu wake kumtuhumu kwamba alidokoa maandazi manne yaliyokuwa ndani ya duka la shule Februari 12 mwaka huu 2023.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ifisi, Dk. Hamis Bakari Ally, amesema wamempokea kijana huyo akiwa na majeraha kichwani, mkononi, goti na miguuni lakini anaendelea vizuri.
Dk. Ally amesema kijana huyo alieleza kupata majeraha baada ya kudokoa maandazi akidai alikuwa na njaa.
Hata hivyo Afisa Elimu mkoa wa Mbeya, Ernest Hinju, amesema maelezo ya awali ya mwanafunzi huyo ni kunyimwa chakula ndipo akaenda kudokoa maandazi manne katika duka la shule, lakini mwalimu aliyefahamika kwa jina la Petro anadai hakumshambulia bali mwanafunzi aliruka dirishani akikimbia adhabu ndipo akapata majeraha hivyo uchunguzi unaendelea kuthibisha mazingira ya tukio hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Kamishana Msaidizi wa Polisi ACP, Benjamin Kuzaga, amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba walimu na walinzi waliohusika na tukio hilo wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi na kwamba baada ya uchunguzi kukamilika taarifa itatolewa.

