Tuesday , 28th Mar , 2023

Umoja wa Afrika umetoa wito wa utulivu na kutoa wito wa kufanyika mazungumzo kufuatia maandamano ya upinzani nchini Kenya ambayo yamegeuka kuwa vurugu na kusababisha vifo vya watu watatu tangu wiki iliyopita.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ameitisha maandamano ya kupinga gharama kubwa ya maisha na kile anachokiita haki ya uchaguzi baada ya uchaguzi wa mwaka jana.

Katika taarifa, Mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat aliwataka  wadau kuwa watulivu na kushiriki katika mazungumzo ili kushughulikia tofauti zozote.

Alisema mwenendo wa uchaguzi wa mwaka jana ulifanikiwa na matokeo kuthibitishwa na Mahakama ya Juu.

"Mwenyekiti anasisitiza mshikamano wa jumla na kuunga mkono juhudi za serikali na watu wa Kenya zinazofanya kazi kuelekea umoja wa kitaifa, amani na utulivu nchini," ilisema taarifa hiyo.

Viongozi wa kidini wa Kenya pia wametoa wito wa mazungumzo yasiyo na masharti kati ya Rais William Ruto na Bw Odinga.