Tuesday , 28th Mar , 2023

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo jumatatu alisema mswada wa kupinga ushoga unaojadiliwa bungeni umebadilishwa kufuatia serikali yake kuingilia kati.

Akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, Bw Akufo-Addo alisema mswada huo sio sera rasmi ya serikali bali umewekwa na wanachama wachache wa kibinafsi.

Alisema mwanasheria mkuu aliwasilisha maoni kwa kamati ya bunge kuhusu "katiba au vinginevyo vya vifungu vyake kadhaa".

"Uelewa wangu... ni kwamba vipengele vikubwa vya muswada huo tayari vimebadilishwa kutokana na kuingilia kati kwa mwanasheria mkuu," alisema bila kutoa maelezo zaidi.

Rais Akufo-Addo alikataa kusema atafanya nini ikiwa mswada huo utapitishwa  na alitumai bunge litazingatia unyeti wa kipengele cha haki za binadamu.

Mapenzi ya jinsia moja tayari yanaadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela nchini Ghana, ambako mitazamo ya ushoga imeenea, lakini rasimu ya sheria hiyo itatoa adhabu ya kifungo cha muda mrefu.

Bw Akufo-Addo awali alizungumzia ndoa za jinsia moja, akisema kamwe haitahalalishwa wakati wa utawala wake.