Tuesday , 9th May , 2023

Jeshi la Polisi Tanzania linatarajia kumuaga rasmi aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Mstaafu Balozi Simon Sirro, Mei 10, 2023 baada ya kustaafu utumishi ndani ya Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria mwezi Machi 2023.

IGP Mstaafu Balozi Simon Sirro

Sherehe hizo za kumuaga IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro zitafanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dares Salaam (DPA) kilichopo Kurasini jijini Dares Salaam kuanzia saa moja asubuhi kwa gwaride maalum la kumuaga ikiwa ni utaratibu wa Jeshi hilo kwa viongozi wa Polisi waliofikia cheo cha Kamishna wa Polisi na Inspekta Jenerali wa Polisi.

IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro amelitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka 30 tangu tarehe 19 Februari 1993 alipojiunga rasmi hadi kustaafu mwezi Machi, 2023 na ni Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Kumi (10) kuliongoza Jeshi la Polisi tangu uhuru na ameliongoza kuanzia tarehe 28 Mei 2017 hadi tarehe 20 Julai 2022.

Wakuu wa Jeshi la Polisi waliomtangulia ni wafuatao ni IGP mstaafu Elangwa Shaidi ambaye ni IGP wa kwanza tangu uhuru aliyeliongoza Jeshi La Polisi Tanzania kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1970.
IGP mstaafu Hamza Azizi (1970 - 1973), IGP mstaafu Samweli Pundugu (1973 - 1975).
IGP Mstaafu Philemon Mgaya (1975 - 1980), IGP Mstaafu Solomon Liani (1980 - 1984), IGP Mstaafu Harun Mahundi (1984 - 1996).
IGP Mstaafu Omari Mahita (1996 - 2006), IGP mstaafu Saidi Mwema (2006 - 2013), na IGP Mstaafu Ernest Mangu (2013 - 2017).