Sunday , 8th Jun , 2025

Rais Samia Suluhu Hassan amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kufuatia ajali ya gari iliyotokea Juni 7, 2025, majira ya saa 1 usiku katika eneo la Mlima Iwambi, Tarafa ya Utengule Usongwe, barabara kuu ya Mbeya-Tunduma. 

Rais Samia Suluhu Hassan

Salamu hizo za rambirambi na pole zimetolewa leo Juni 8, 2025, na kueleza kuwa ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 830 EDP/T 148 CID lililokuwa limebeba shehena ya unga kutoka Dar es Salaam kuelekea Zambia, lililogonga kwa nyuma magari mawili namba T 257 DVP aina ya Mitsubishi Rosa na T 185 DMF aina ya Toyota Lite Ace na hatimaye kuanguka katika bonde la Mto Mbalizi. 

Chanzo cha ajali kinasadikiwa kuwa ni uzembe wa dereva wa lori kushindwa kulimudu gari kwenye mteremko. 

"Katika ajali hiyo, watu 28 wamepoteza maisha wakiwemo wanawake 12 (kati yao watoto wawili) na wanaume 16 (kati yao watoto wawili). Hadi sasa, miili 19 imetambuliwa na tisa haijatambuliwa. Aidha, watu nane (wanaume sita na wanawake wawili) wamejeruhiwa. Rais Dkt. Samia anatoa wito kwa madereva wote nchini kuzingatia sheria za usalama barabarani," imeeleza taarifa hiyo 

Aidha taarifa ya Rais Samia imeongeza kuwa, "Rais Dkt. Samia anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia za marehemu na wote walioguswa na msiba huu mkubwa katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, Mwenyezi Mungu awape majeruhi nafuu ya haraka na azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amin,"