
Serikali ya China itawapa wazazi ruzuku ya kila mwaka ya yuan 3,600 sawa na Shilingi 1,285,000 kwa kila mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitatu, kama hatua ya kuchochea ongezeko la viwango vya uzazi ambavyo vimeshuka nchini humo.
Vyombo vya habari vya serikali ya Beijing vimetangaza Jumatatu, Julai 28 kuwa ruzuku hiyo (sawa na dola 500 za Marekani au euro 429) itaanza kutolewa kuanzia mwaka huu, huku ruzuku ya kiasi fulani ikitolewa kwa watoto walio chini ya miaka mitatu waliozaliwa kabla ya mwaka 2025.
Idadi ya watu nchini China imekuwa ikipungua kwa miaka mitatu mfululizo, na Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa inaweza kushuka kutoka watu bilioni 1.4 wa sasa hadi milioni 800 kufikia mwaka 2100.
Viwango vya ndoa nchini China pia vimefikia kiwango cha chini kabisa katika historia. Wenzi wachanga wamekuwa wakiahirisha kupata watoto kutokana na gharama kubwa ya kuwalea watoto na wasiwasi kuhusu maendeleo ya kazi zao.
Zaidi ya serikali 20 za ngazi ya mikoa nchini China sasa zinatoa ruzuku kwa ajili ya malezi ya watoto. Wachambuzi wamesema ruzuku hizo ni hatua chanya, lakini wameonya kuwa haziwezi kuwa suluhisho pekee la kugeuza mwelekeo wa kupungua kwa idadi ya watu nchini China au kuchochea matumizi ya ndani ambayo yamedorora.