
Makandarasi wameaswa kufanya kazi kwa viwango na ubora unaotakiwa kwa kuzingatia makubaliano katika mikataba ya utekelezaji wa miradi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya Usimamizi wa Mikataba (Contracts Management) ya siku tatu yenye lengo la kuwajengea uwezo Makandarasi wazawa yanayofanyika kuanzia leo Mkoani Iringa, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori, amesema kuwa lengo la kufanya mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa Makandarasi na kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia wajibu wao pamoja na haki zao kama zinavyoainishwa katika mikataba ya kazi zao.
“Kupitia mafunzo yatakayotolewa naamini mtajifunza mada mbalimbali ikiwemo kuzijua na kuzingatia haki na wajibu wenu kwa kuzingatia mikataba ya miradi mbalimbali mnayotekeleza”, alisema Mhandisi Nkori.
Mhandisi Nkori ameongezea kuwa, ukandarasi ni biashara ya kimkataba hivyo ni wajibu wa kila Mkandarasi kuwa na ujuzi wa usimamizi wa mikataba ili kujua haki zake na kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kuepuka kufanya biashara hiyo kwa upendeleo au kwa maslahi bianfsi bali wazingatie maadili ya taaluma zao.
"Biashara ya ukandarasi ni ya kitaalamu, lakini wapo baadhi ya Makandarasi wamekuwa wakiiendesha kinyume na misingi ya taaluma. Mkandarasi unapoingia mkataba, haijalishi unafahamiana na nani unatakiwa kutekeleza wajibu wako ipasavyo ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria," alisema Mhandisi Nkori.
Aidha Mhandisi Nkori, alitoa rai kwa Makandarasi kuzichangamkia fursa mbalimbali za mafunzo yanayoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo ili kujengewa uwezo mzuri utakaowasaidia wakati wa utendaji wa kazi zao.
Mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa 10 hapa nchini wakiwemo Makandarasi na Waajiri.