
Taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu zimetakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa Tume na taasisi na asasi hizo leo Julai 30, 2025 jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa katika kipindi cha uchaguzi Tume itafanya kazi kwa karibu na taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura.
Jaji Mwambegele ameongeza kuwa wakati wa kampeni uzoefu unaonesha kuwa kunakuwa na joto la kisiasa linatokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa, hivyo ameziasa taasisi na asasi hizo kutumia nafasi yao kuwaelimisha wananchi ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.
Baadhi ya wawakilishi wa taasisi na asasi hizo wamesema wamejipanga rasmi kutoa elimu ya mpiga kura haswa kwa vijana wanaotarajia kupiga kura kwa mara ya kwanza. Wamesisitiza kuwa watatoa elimu kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Tume.