Thursday , 31st Jul , 2025

Dkt. Jafo amesema eneo la zaidi ya hekta 1,000 linatarajiwa kuwa kitovu kikuu cha viwanda nchini, likiwa na uwekezaji wa zaidi ya Dola bilioni 3 za Kimarekani, ambapo zaidi ya viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amemsifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua yake ya kihistoria ya kuweka jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda ya Kwala (Kwala Industrial Park), akisema ni hatua kubwa kuelekea ndoto ya Tanzania ya viwanda.

Akizungumza mbele ya umati wa wananchi, wawekezaji na viongozi wa serikali katika tukio hilo maalum, Dkt. Jafo alisema eneo hilo la zaidi ya hekta 1,000 linatarajiwa kuwa kitovu kikuu cha viwanda nchini, likiwa na uwekezaji wa zaidi ya Dola bilioni 3 za Kimarekani, ambapo zaidi ya viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa.

Dkt. Jafo alibainisha kuwa kupitia mradi huo mkubwa, jumla ya ajira 250,000 zinatarajiwa kupatikana – ajira 50,000 za moja kwa moja kwa vijana wa Mkoa wa Pwani, na nyingine 200,000 zisizo za moja kwa moja, jambo ambalo linakwenda kuchochea uchumi wa watu wa kawaida na taifa kwa ujumla.

Waziri Jafo ameendelea kupongeza uongozi wa Rais Samia kwa juhudi kubwa katika kuimarisha sekta ya viwanda, akisema chini ya uongozi wake sekta hiyo imepata msukumo mkubwa na mwelekeo thabiti wa maendeleo.

Kongani ya Kwala inatarajiwa kuwa kitovu cha kimkakati cha viwanda barani Afrika, kwa kuzingatia ukubwa wa eneo lake, miundombinu ya kisasa inayojengwa, na uwepo wa njia muhimu za usafirishaji – ikiwemo reli ya kisasa (SGR), barabara kuu na ukaribu wake na Bandari ya Dar es Salaam.