Thursday , 31st Jul , 2025

Kikosi tawala nchini Myanmar kimetangaza leo Alhamisi, Julai 31, kuondolewa kwa hali ya hatari katika nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia 

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni kuelekea uchaguzi wa mwezi Desemba, ambao umesusiwa na makundi ya upinzani na kulaaniwa na waangalizi wa kimataifa.

Utawala wa kijeshi nchini Myanmar umesitisha hali ya hatari katika nchi hiyo ya Kusini-mashariki mwa Asia siku ya Alhamisi, Julai 31, miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu ambao makundi ya upinzani yananuia kuususia, uchaguzi unaoshtumiwa na waangalizi wa kimataifa.

Msemaji wa utawala wa kijeshi Zaw Min Tun amesema Hali ya hatari imesitishwa leo, katika ujumbe uliotumwa kwa vyombo vya habari, na hivyo kumaliza hali ya dharura iliyotangazwa wakati jeshi lilipopindua serikali iliyochaguliwa ya kiraia ya mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi Februari 2021.

Kutangazwa kwa hali ya hatari kulizusha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu nchini Myanmar. 

Hatua hii ya kipekee ilimpa kiongozi wa utawala wakijeshi Min Aung Hlaing mamlaka ya juu juu kwenye Bunge, serikali na mahakama.

Lakini hivi karibuni kiongozi wa Myanmar alisema kuwa uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mwezi wa Desemba na Januari, unaweza kuleta suluhu la mzozo huo, kwani maeneo makubwa ya Myanmar yanashikiliwa na makundi ya waasi na yako nje ya uwezo wa utawala wa kijeshi.

Wapinzani, wakiwemo wabunge wa zamani waliotimuliwa katika mapinduzi hayo, wameapa kususia uchaguzi huo, ambao mtaalamu wa Umoja wa Mataifa aliutaja mwezi uliopita kuwa ni "ujanja" unaolenga kuhalalisha kuendelea kwa utawala wa kijeshi.

Siku ya Jumatano serikali ya Myanma ilitangaza kwamba imetunga sheria inayotoa hukumu ya kifungo jela kwa wakosoaji au waandamanaji wanaopinga uchaguzi mkuu.