Monday , 4th Aug , 2025

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia watuhumiwa 55 kwa makosa mbalimbali ya jinai.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwezi Julai Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi SACP Kaster Ngonyani amesema watuhumiwa 19 wamekamatwa wakiwa na pikipiki 3 moja ikiwa haina namba za usajili. Ngionyani amezitaja pikipiki hizo kuwa ni Sanlg MC. 120 CVC aina ya Kinglion na MC.113 BWJ aina ya Sanlg.

Watuhumiwa wengine 13 wamekamatwa wakiwa na pombe haramu ya moshi maarufu kwa jina la gongo kiasi cha lita 85, huku watuhumiwa 6 wakikamatwa na dawa za kulevya aina ya bangi kiasi cha kilogramu 18 na kete 27.

Kamanda Ngonyani amewataja watuhumiwa wengine 12 kuwa wamekamatwa wakiwa na nyara za serikali ikiwemo pembe moja ya mnyama pofu pamoja na kilo 41 ya wanyama pori ambao ni  twiga, ngiri, nguruwe pori, nyati na pofu.

Katika hatua nyingine watuhumiwa 10 wamekamatwa wakiwa na ngo'mbe 5 na mbuzi waliowaiba baada ya kuvunja zizi. Aidha mtuhumiwa mmoja amekamatwa akiwa na silaha moja aina ya Gobore huku silaha 2 aina ya gobore zimesalimishwa nje ya ofisi ya mwenyekiti wa kijiji cha Tukoma Wilaya ya Mpanda. 

Upande wa Makosa ya usalama barabarani jumla ya makosa 3,177 ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani walikamatwa na mtuhumiwa mmoja kufikishwa mahakamani. Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili mkoa wa Katavi uendelee kuwa salama.