
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wazazi na walezi kote nchini kuhakikisha wanawapeleka vijana wao kupata mafunzo ya ufundi stadi yanayoratibiwa na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza mara baada ya kukagua karakana za kujifunzia zilizopo katika Chuo cha VETA wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha miundombinu ya vyuo vya ufundi stadi pamoja na kuratibu programu za mafunzo ili kuhakikisha vijana wanapata stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na baadaye.
“Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa na ujuzi. Mafunzo ya VETA na yale yanayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu yanawawezesha vijana wetu kuajiriwa au kujiajiri wenyewe, na hii ni hatua kubwa ya maendeleo kwa familia zao na Taifa kwa ujumla,” amesema Waziri Mkuu.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia alitembelea eneo linalojengwa hosteli kwa ajili ya timu ya mpira wa miguu ya Namungo sambamba na kukagua uwanja wa michezo wa Kassim Majaliwa uliopo Ruangwa ambao unatarajiwa kuwekwa viti katika majukwa.