Wednesday , 13th Aug , 2025

Viongozi wa Ulaya pamoja na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine watafanya mazungumzo Ijumaa kwa njia ya mtandao na Rais Donald Trump wa Marekani, kabla ya mkutano wake na Vladimir Putin siku hiyo

Viongozi hao wananuia kumshawishi Trump kuheshimu maslahi ya Kyiv, atakapokutana na Rais Vladimir Putin siku ya Ijumaa huko Alaska kujadili vita vya nchini Ukraine.

Zelensky anakwenda mjini Berlin kuungana na Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani atakayeongoza mazungumzo hayo

Merz aidha amewaalika wakuu wa mataifa ya Ufaransa, Uingereza na wengine wa Ulaya pamoja na wakuu wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya NATO, kushiriki mazungumzo hayo.

Watazungumza na Rais Trump na Makamu wake JD Vance, kwenye duru ya pili ya mazungumzo hayo.

Mazungumzo hayo ya Ijumaa yamepangwa kufanyika bila ya Zelensky, hatua inayoibua wasiwasi kwamba huenda Ukraine ikalazimishwa kuingia kwenye makubaliano magumu, ikiwa ni pamoja na kuachilia ardhi yake, huku Ulaya ikisisitiza haki ya Ukraine ya kuchagua mustakabali wake.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema nchi yake na washirika wake ni lazima washirikiane kuishinikiza Urusi kumaliza uvamizi wake nchini mwake.