
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ameomba kwa niaba ya chama hicho kukutana na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dharura ili kuwasilisha maoni ya wadau mbalimbali juu ya changamoto ufumbuzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo August 26, 2025 Jijini Dar es salaam, Rais wa TLS Boniface Mwabukusi amesema lengo la kuomba kikao hicho ni kulifanya Taifa kuingia kwenye uchaguzi likiwa na amani na kurejesha imani ya Wananchi kwenye Mamlaka za uchaguzi ambazo zinaonekana kutoaminika miongoni mwa wengi.
“Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na migawanyika ya kisiasa, kidini na kikabila. Hatuwezi kuyaonea aibu. TLS imewasiliana na Ofisi ya Rais ili kuwasilisha maazimio ya Wadau, tukipata nafasi ya kukutana na Rais, tutatoa ushauri wa hatua za haraka za kuchukuliwa ili kurudisha imani ya Wananchi na kuhakikisha uchaguzi unakuwa shirikishi, shindani na wenye uhalali wa kisiasa”.
Ameongeza kuwa hadi sasa hawajapata majibu kutoka Ofisi ya Rais na kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa TLS kuwasilisha maoni hayo, kwani kuna haja ya kusimama imara kama Taifa kwa kusikilizana na kuelewana kwenye masuala muhimu ya kitaifa kama suala la uchaguzi mkuu.
Aidha, TLS imeishauri Serikali kupitia kwa DPP kumwachilia huru kwa kuziondoa Mahakamani kesi zinazomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu akisema kesi hizo ni za kisiasa. Akizungumzia utekaji, Mwabukusi amesema, "Watu wametekwa na tunaona. Kwa sasa simuoni Mdude na sijui yupo wapi, waliomchukua wanajulikana walipo na watu wapo kimya tu, yeye amekuwa kama mbuzi wa kafara. Na tukija tukaomba serikali ibadilike tuna nia njema na siyo kuipinga Serikali”.