
Mitetemeko miwili mikubwa imeshuhudiwa tena mashariki mwa Afghanistan katika muda wa saa 12, kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti cha Ujerumani cha Sayansi ya Jiolojia (GFZ) na kusababisha hofu ya vifo na uharibifu zaidi leo Ijumaa katika eneo ambalo takriban watu 2,200 wamefariki katika tetemeko la ardhi lililotokea ndani ya siku nne.
Matetemeko mawili ya ardhi katika siku chache zilizopita yaliharibu sehemu kubwa ya taifa hilo la Asia Kusini, lililokandamizwa na vita, umaskini na kupungua kwa misaada. Utawala wa Taliban umekadiria vifo 2,205 na majeruhi 3,640 kufikia jana Alhamisi.
Tetemeko la ardhi la kwanza lililotokea Jumamosi la kipimo cha 6 katika kipimo cha Richter, dakika chache kabla ya saa sita usiku Jumapili, lilikuwa mojawapo ya maafa makubwa zaidi nchini Afghanistan, na kusababisha uharibifu katika majimbo ya Nangarhar na Kunar likipiga kwa kina cha kilomita 10.
Tetemeko la pili la ukubwa wa 5.5 siku ya Jumanne lilisababisha hofu na kutatiza juhudi za uokoaji huku likipelekea mawe kutoka milimani na kufunga barabara kuelekea vijiji vya maeneo ya mbali. Kutokana na nyumba nyingi kujengwa kwa mawe, na mbao, baadhi ya familia zililazimika kukaa mahali pa wazi badala ya kurudi nyumbani ikiwa ni tahadhari dhidi ya matetemeko ya baadaye.
Umoja wa Mataifa, ambao umesema pesa za kuwasaidia waathiriwa wa tetemeko zitaisha hivi karibuni, unapanga kuzindua ombi la dharura la fedha na umetoa dola milioni 10, zaidi ya fedha taslimu zilizotangazwa na mataifa tajiri, huku wengine wakituma msaada kama vile mahema.
Manusura katika eneo linalokumbwa na tetemeko la ardhi wanahangaika kutafuta huduma za kimsingi huku Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yakionya kuhusu hitaji kubwa la fedha, chakula, vifaa vya matibabu na makazi, huku Shirika la Afya Duniani likitafuta fedha kiasi cha dola milioni 4 kwa ajili ya msaada.