Friday , 3rd Oct , 2025

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametoa onyo kali kwa Marekani kuhusu uwezekano wa ongezeko la vita kati ya Urusi na Ukraine endapo Washington itatoa makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk kwa Kiev.

Putin amesema kutolewa kwa makombora hayo kutamaanisha Marekani imejiingiza moja kwa moja katika vita vyake na Ukraine. Ameielezea hali hiyo kuwa hatari akifafanua nguvu ya makombora hayo na uwezo wake wa kuidhuru Urusi.

Rais Vladimir Putin pia amesema utoaji wa makombora hayo hautabadilisha mwelekeo wake katika uwanja wa vita lakini bila shaka utayatia doa mahusiano yake na Marekani na kufungua nafasi ya mgogoro kutanuka zaidi.
Amesisitiza kuwa Urusi sio dhaifu na iko imara katika maamuzi yake.

Putin amesema kuwa Historia ya Urusi  imedhihirisha kwamba udhaifu haukubaliki, kwa sababu unajenga majaribu..
Amesema kuwa Kuna fikra kwamba suala lao lolote ni lazima lisuluhishwe kwa kutumia nguvu. 
Ameongeza kuwa Urusi haitaonyesha udhaifu kamwe au kutokuwa na maamuzi sahihi"

Kiongozi huyo wa Urusi amesema nchi yake itaimarisha mfumo wake wa kujikinga na makombora ili kuzuwia aina yoyote ya makombora itakayovurumishwa nchini mwake. 

Matamshi yake yamekuja baada ya ripoti za vyombo vya habari kwamba Marekani inafikiria kutoa makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk kwa Ukraine.