Katika kuboresha upatikanaji wa umeme Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema makandarasi watakaoshindwa kutimiza majukumu yao au kufanya uzembe watachukuliwa hatua za kisheria ili kuendana na kasi ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya umeme kwa wakati.
Akizungumza Novemba 22, 2025 jijini Dodoma katika kikao cha tathmini na kupanga mikakati, Waziri Ndejembi amepongeza mageuzi yanayofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), katika kuboresha upatikanaji wa umeme yameongeza imani na fursa za kiuchumi kwa wananchi huku akiwataka watendaji wa Tanesco kuongeza kasi na ubunifu katika kuwaunganishia wananchi umeme, sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Misheni 300.
“Nawapongeza Tanesco kwa kazi nzuri, lakini bado tunahitaji kuongeza ubunifu. Tukishirikiana na wadau, tutafikia lengo la kuwaunganishia wateja milioni 1.7 kwa mwaka,” amesema Ndejembi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba ameishukuru Serikali kwa kuwekeza kwenye miradi ya nishati, huku Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Felchesmi Mramba, akisema Tanesco inatekeleza miradi kwa viwango vya kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, amesema ndani ya siku 100, miradi muhimu ikiwemo wa umeme wa jua wa Kishapu uliofikia asilimia 83, itakamilika.

