Monday , 29th Dec , 2025

Mazoezi hayo ambayo yanayodhaniwa kuwa yanaweza kuendelea hadi kesho Disemba 30, yanahusisha vikosi vya anga, majini na ardhini, huku yakilenga kuonyesha uwezo wa kijeshi wa China na msimamo wake kuhusu suala la Taiwan, ambayo Beijing inaiona kama sehemu ya eneo lake.

China imeanzisha tena mfululizo wa mazoezi makubwa ya kijeshi katika maeneo yanayozunguka kisiwa cha Taiwan leo Jumatatu Disemba 29, hatua inayoongeza mvutano wa kisiasa na kiusalama katika eneo la Asia Mashariki.

Mazoezi hayo ambayo yanayodhaniwa kuwa yanaweza kuendelea hadi kesho Disemba 30, yanahusisha vikosi vya anga, majini na ardhini, huku yakilenga kuonyesha uwezo wa kijeshi wa China na msimamo wake kuhusu suala la Taiwan, ambayo Beijing inaiona kama sehemu ya eneo lake.

Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la China, mazoezi hayo yanalenga kuimarisha utayari wa kivita na kuzuia kile walichokitaja kama harakati za kujitenga za Taiwan. Hatua hiyo imekuja kufuatia matamko na mienendo ya kisiasa ambayo China inadai inahatarisha mamlaka yake na umoja wa taifa.

Kwa upande wake, Taiwan imelaani vikali hatua ya China, ikisema ni kitendo cha kutishia amani na uthabiti wa kikanda. Viongozi wa Taiwan wamesisitiza kuwa kisiwa hicho kiko tayari kujilinda na kulinda mfumo wake wa kidemokrasia dhidi ya vitisho vyovyote vya nje.

Rais wa Taiwan amesema kuwa wananchi wa kisiwa hicho wamejizatiti kusimamia uhuru wao wa kisiasa na haki za kidemokrasia, akiongeza kuwa jeshi la Taiwan liko katika hali ya tahadhari ya juu. Aidha, amezitaka nchi rafiki kuendelea kuunga mkono juhudi za kulinda amani na demokrasia katika eneo hilo.

Mazoezi hayo ya kijeshi yameibua wasiwasi mkubwa kimataifa, huku mataifa kadhaa yakihimiza pande zote kujizuia na kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo ya amani. Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaonya kuwa mvutano unaoendelea kati ya China na Taiwan unaweza kuwa na athari kubwa kwa usalama wa kikanda na uchumi wa dunia.