Mashambulizi ya Marekani usiku wa Ijumaa, Januari 2 kuamkia Jumamosi, Januari 3, na kutekwa nyara kwa Nicolas Maduro, yameongeza mvutano nchini Venezuela kutokana na kupelekwa kwa makundi ya wanamgambo wanaounga mkono utawala wa Maduro katika mitaa ya Caracas.
Hayo yanajiri wakati hali ya hatari ikiwa tayari imetangazwa nchini humo, ikiruhusu kukamatwa kwa mwandamanaji yeyote anayesherehekea operesheni ya Marekani. Sheria hiyo ilipitishwa mnamo mwezi Septemba na rais anayeshikiliwa na Marekani, Nicolás Maduro.
Makundi ya wanamgambo wenye silaha yamesambazwa katika mitaa ya Caracas ili kudumisha utulivu. Angalau watu wawili tayari wamekamatwa kwa kusherehekea kutekwa nyara kwa Nicolas Maduro.
Katika kitongoji cha Boleita, mashariki mwa Caracas, wanaume wenye silaha wamekuwa wakizunguka kwa siku kadhaa, wakiwa na bunduki ndefu kwa mujibu wa wakazi wa jiji hilo.
Vizuizi vya barabarani pia vimewekwa kwenye barabara kuu. Wanaume wanaojifunika nyuso zao wamekuwa wakiangalia vitambulisho, kukagua magari, na hata simu.
Tangu kukamatwa kwa Nicolas Maduro nchini Venezuela, upinzani katika Bunge la Marekani (chama cha Democratic) umemshumu Donald Trump kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ya kikatiba, ukisema kwamba rais wa Marekani alipaswa kushauriana na kuarifu Bunge kabla ya kuanzisha shambulio nchini Venezuela.
Baada ya kukana hatia katika mahakama ya New York Jumatatu, Januari 5, Rais aliyeondolewa madarakani Nicolás Maduro na mkewe bado wako kizuizini nchini Marekani.



