Serikali kuiuzia Dangote gesi asilia kwa miaka 20

Jumatatu , 20th Aug , 2018

Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini TPDC, kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake Mhandisi Kapuulya Musomba, limesaini mkataba wa miaka 20 wa kukipatia kiwanda cha saruji cha Dangote, gesi asilia kama nishati kwa ajili ya kuzalisha saruji.

Kiwanda cha Dangote.

Kufuatia makubaliano hayo yaliyosainiwa jijini Dar es salaam hii leo, kiwanda cha Dangote kitaacha matumizi ya nishati ya mafuta katika uzalishaji na kwamba mchakato wa kuhama kutoka matumizi ya mafuta kwenda ya gesi utachukua kati ya siku 30 hadi siku 45 kuanzia sasa.

Hivi karibuni kumekuwa na uhaba wa saruji katika soko ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda Mh. Charles Mwijage, moja ya sababu ni kupungua kwa uzalishaji wa kiwanda cha Dangote hivyo kusainiwa kwa makubaliano hayo kutasaidia kupunguza kuadimika kwa bidhaa ya saruji katika siku za usoni.

Mradi wa gesi asilia na iliyosindikwa Tanzania (TGP) ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya ujenzi wa miundombinu katika historia ya Tanzania matumizi ya gesi iliyopo nchini yataongeza uwezo wa nchi wa kusafirisha nje rasilimali hiyo na kuboresha miundombinu ya ndani.