Jumatano , 9th Sep , 2020

Wafanyabiashara katika fukwe za Coco jijini Dar es Salaam wamesema kuwa hali ya biashara imeanza kurejea tofauti na miezi mitatu iliyopita wakati wa janga la Covid 19 lililosababisha watu wengi kufanya kazi wakiwa nyumbani na hivyo kupunguza idadi wa wateja katika eneo hilo.

Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo la Coco Beach akiandaa sharobati ya miwa.

Wakizungumza na EATV wafanyabiashara hao Bernard Mwinuka na  Ashrafu Mwalami wamesema kuwa, kwa sasa hali imechangamka kwani Watu wameanza kufika katika fukwe hizo kwa wingi tofauti na kipindi cha miezi mitatu ambapo wamefafanua kupata hasara kiasi kilichosababisha wengi wao kupoteza mitaji yao.

Wamesema licha ya wateja wao wengi kuwa ni raia wa Tanzania lakini eneo hilo lililikuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka nje ya nchi ambao hupendelea kutembelea fukwe hizo pamoja na kupata huduma zitolewazo eneo hilo ikiwa ni pamoja na kitoweo cha mihogo na bidhaa za kitamaduni.

“Kipindi cha mlipuko wa Corona hali ilikuwa mbaya, ukweli tunashukuru jitihada zilizofanywa na serikali katika kuhakikisha inadhibiti maambukizi ya virusi hivyo ikiwa ni pamoja na mikakati ya kujikinga ikiwemo unawaji wa mikono pamoja na uvaaji wa barakoa"amesema Mwinuka.