Jumatatu , 5th Jan , 2026

“Hatukuwahi kuamini kuwa kuna nchi yoyote inayoweza kujifanya kuwa polisi wa dunia, wala hatukubali taifa lolote kudai kuwa hakimu wa dunia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, amesema Beijing haiwezi kukubali nchi yoyote kujichukulia jukumu la kuwa hakimu wa dunia baada ya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro.

Wang ametoa kauli hiyo siku ya Jumapili Januari 4 kwa mwenzake wa Pakistan, Ishaq Dar, wakati wa kikao chao mjini Beijing akirejelea matukio aliyoyaita kuwa ya ghafla nchini Venezuela bila kuitaja Marekani moja kwa moja.

“Hatukuwahi kuamini kuwa kuna nchi yoyote inayoweza kujifanya kuwa polisi wa dunia, wala hatukubali taifa lolote kudai kuwa hakimu wa dunia. Ukuu wa mamlaka na usalama wa nchi zote unapaswa kulindwa kikamilifu chini ya sheria za kimataifa,” aliongeza mwanadiplomasia mkuu huyo wa China katika kauli zake za kwanza tangu picha za Rais Nicolas Maduro (63) akiwa amefungwa pingu na kufunikwa macho zilipoonekana siku ya Jumamosi.

Maduro kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha mahabusu mjini New York akisubiri kufikishwa mahakamani leo Jumatatu kwa tuhuma za biashara ya dawa za kulevya.

China imejitanabaisha kuwa na nia ya kuwa nguzo muhimu ya diplomasia ya kimataifa, lengo ambalo ililieleza kwa uwazi zaidi mwaka 2023 baada ya kufanikisha kwa mshangao maridhiano kati ya Saudi Arabia na Iran.

Wachambuzi wanasema mafanikio ya China katika kukabiliana uso kwa uso na Marekani kwenye mazungumzo ya kibiashara yamezidi kuimarisha kujiamini kwa Beijing.

Kauli ya Rais Donald Trump kwamba Marekani itasimamia serikali ya Venezuela kwa muda imeuweka pagumu ushirikiano wa kimkakati wa kina wa kudumu katika nyakati zote ambao Beijing na Caracas waliufikia mwaka 2023, ukiashiria takriban miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Qiu Xiaoqi, afisa wa serikali ya China aliyearifiwa kuhusu mkutano kati ya Maduro na mwakilishi maalum wa China katika masuala ya Amerika ya Kusini na Karibiani, saa chache kabla ya kukamatwa kwa Maduro ameitaja hatua ya Marekani kuwa ni kubwa kwa China.

China, ambayo ni uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, imekuwa ikiiwezesha Venezuela kuendelea kiuchumi tangu Marekani na washirika wake walipoimarisha vikwazo mwaka 2017, ikinunua bidhaa zenye thamani ya takribani dola bilioni 1.6 mwaka 2024.

Takriban nusu ya manunuzi yote ya China nchini Venezuela yalikuwa mafuta ghafi, kulingana na takwimu za forodha, huku makampuni makubwa ya mafuta yanayomilikiwa na serikali ya China yakiwa yamewekeza karibu dola bilioni 4.6 nchini Venezuela kufikia mwaka 2018.