11 kizimbani wakidaiwa kuwauwa Askari 2

Alhamisi , 16th Jan , 2020

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma imewapandisha kizimbani washtakiwa 11 na  kuwasomea shitaka la kuwaua Askari Polisi 2 huku mmoja wao kukatwa sehemu za siri katika Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, wakati wa mapambano yaliyotokea mwaka 2018 kati ya Askari na wananchi.

Sheria

Kesi hiyo jinai namba 15 ya mwaka 2018 inayowakabili washtakiwa 11 ni makosa mawili ya kuuwa kwa kukusudia Askari wawili Inspecta Ramadhani Hamis pamoja na Mohamed Zengo ambapo imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Gadiel Maliki.

Akisoma maelezo ya kesi hiyo Mwendesha Mashtaka wa Serikali Robert Magige,  amesema kuwa watatumia Mashahidi 37 katika kesi hiyo wakiwemo Maaskari waliokuwa katika operesheni hiyo ambao wengine walishuhudia tukio hilo..

Ameongeza kuwa maelezo ya awali ya washtakiwa yanabainisha kuwa baada ya kusikia katazo la kuishi hifadhini walihamasishana kupambana na Askari wakiwa karibu wananchi 1000 waliojigawa makundi makundi.