Jumatano , 1st Oct , 2025

"Juhudi za uokoaji kwa sasa zinafanywa kwa mikono kwa kuchimba mashimo ili kuwaondoa manusura,"

Takriban watu 91 wanahofiwa kuwa bado wamenasa chini ya vifusi vya jengo kufuatia kuanguka kwa shule nchini Indonesia, hii ni kwa mujibu wa mamlaka ya serikali nchini humo.

Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Maafa la Indonesia, BNPB, limeripoti takwimu za hivi punde jana Jumanne jioni, na kurekebisha idadi hiyo kutoka kuwa makadirio ya watu 38 hadi watu 91. Shirika hilo lilisema takriban watu sita bado wako hai chini ya vifusi, ambapo wamenaswa kwa karibu siku mbili.

"Juhudi za uokoaji kwa sasa zinafanywa kwa mikono kwa kuchimba mashimo ili kuwaondoa manusura," BNPB ilisema katika taarifa kwenye mtandao wa Facebook, ikibainisha kuwa matumizi ya vifaa vizito yanaweza kusababisha kuanguka zaidi kwa jengo hilo.

"Timu ya pamoja (ya utafutaji na uokoaji)  imegundua dalili za watu sita ambao bado wako hai katika sehemu moja. Kupitia mupenyo uliopo, waokoaji wameweza kutoa chakula na maji waathirika," shirika hilo lilisema.

Idadi kamili ya waliofariki kutokana na kuporomoka kwa jengo la shule hiyo imefikia watatu na karibu majeruhi 100, ingawa takwimu hazihesabii watu ambao bado wamenaswa. Kati ya waliojeruhiwa, 70 wameruhusiwa, na 26 wamesalia hospitalini kwa mujibu wa shirika hilo.

Zaidi ya wafanyakazi 300 wa uokoaji kutoka BNPB, wanajeshi na polisi wa kitaifa wametumwa kwenye eneo la ajali katika Shule ya Bweni ya Al Khoziny ya Kiislamu huko Sidoarjo, Java Mashariki, ambayo ilianguka Jumatatu alasiri wakati wanafunzi  hasa wavulana na wafanyakazi wakiwa katika maombi.

"Iwapo tathmini itahitimisha kuwa hakuna manusura zaidi, awamu inayofuata itahusisha matumizi ya vifaa vizito kuwaokoa waathiriwa waliofariki ambao bado wamenaswa," shirika hilo lilisema. Mamlaka inasema nguzo za msingi za shule hiyo ziliacha kufanya kazi wakati kazi ya ujenzi isiyoidhinishwa ikiendelea kwenye ghorofa ya juu.