Ijumaa , 13th Sep , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka mamlaka husika ziwachukulie hatua za kinidhamu watu ambao hawakutekeleza majukumu yao katika tukio la ajali ya moto, iliyotokea Agosti 11, 2019 mkoani Morogoro, na kusababisha vifo vya watu 104.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Bungeni, wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma.

"Baada ya tukio hilo la kusikitisha 12 Agosti, 2019, niliunda Kamati kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo, iliyosababisha vifo majeruhi na uharibifu wa mali." amesema Waziri Mkuu

"Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu, kabla na baada ya ajali kutokea." ameongeza.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru Madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na wadau wote ambao walishiriki kuokoa maisha ya waathirika wa ajali hiyo tangu ilipotokea.