Jumapili , 1st Sep , 2019

Hospitali ya Taifa ya Muhmbili imesema itaanza kutumia vipimo va DNA kwa ajili ya kuwatambua marehemu waliofariki kwenye ajali iliyotokea Kibiti ambapo kwa sasa miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti.

Ajali ya gari la kampuni ya Dangote

Muhimbili wamesema kuwa miili hiyo ni ya watu wazima wanne na mtoto mmoja, ambayo imeungua sana kiasi cha utambuzi wake kuwa mgumu, na tayari Hospitali ya Taifa Muhimbili imefanya uchunguzi na kuchukua sampuli kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Forensic Pathology pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali.

"Hivyo tunawaomba ndugu wa karibu wa marehemu hawa Baba, Mama na mtoto, kujitokeza kuanzia kesho 2 Septemba, 2019 saa mbili asubuhi ili kuchukuliwa sampuli na Mkemia Mkuu wa Serikali ili kusaidia kufanya uchunguzi", amesema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Muhimbili, Aminiel.

Mapema jana Watu wanne waliokuwa wakisafiri kwa gari ya Dangote iliyokuwa ikitokea Dar es salaam, kuelekea Mtwara wameteketea kwa moto baada ya gari waliokuwa wakisafiria kugongana na gari ndogo eneo la Shule ya Sekondari Kibiti, Rufiji mkoani Pwani, ambapo gari lilipinduka na kuangukiwa na nguzo ya umeme iliyosababisha gari kuwaka moto.