Alhamisi , 9th Mar , 2023

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limetangaza nafasi za kujiunga na jeshi hilo kwa vijana Watanzania wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi Shahada ya Uzamili ambao wamemaliza mkataba wa mafunzo ya kujitolea JKT na kurudishwa majumbani.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, na kusema sifa za kujiunga ni lazima kijana awe na miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha nne hadi cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu pia awe na afya nzuri na akili timamu.

"Awe Mtanzania mwenye tabia na nidhamu nzuri, hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani na kufungwa, awe na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na taaluma, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, asiwe ameoa au kuolewa" amesema Luteni Kanali Ilonda

Aidha Luteni Kanali Ilonda amesisitiza, "Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya jeshi, Dodoma kuanzia tarehe ya tangazo hili yaani leo hadi tarehe 20 Machi, 2023 yakiambatishwa na nakala ya kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala ya cheti cha JKT na namba ya simu ya mkononi ya mwombaji".