Jumatano , 22nd Mei , 2019

Tafiti zinaonesha zaidi ya wanawake 800 Duniani hupoteza maisha kila siku kutokana na matatizo yatokanayo na ujauzito ambapo 20 kati yao wananapata majeraha au ulemavu na moja ya majeraha makubwa wakati wa kujifungua ni tatizo la fistula ya uzazi. 

Picha wa wakina mama wanaotibiwa Fistula katika hospitali ya CCBRT jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo Mwakilishi kutoka Shirika la idadi ya watu Duniani (UNFPA) Felister Bwana amesema kuwa mimba za utotoni, huduma duni za afya ni chanzo kikubwa cha ugonjwa huo kwa nchi za kiafrika.

"Inakadiriwa kwamba wanawake na wasichana zaidi ya milioni mbili wanaishi na tatizo la fistula duniani na hasa chini ya jangwa la Sahara", amesema Felister.

Www.eatv.tv imezungumza na baadhi ya wanawake wenye tatizo la Fistula ambao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya CCBRT na wametoa ushuhuda wa namna walivyonyanyapaliwaa huku wakieleza hali zao kwa sasa baada ya kupata matibabu, Rehema Malugu kutoka mkoani Mara anaeleza kuwa ameishi na ugonjwa huo kwa miaka ishirini.

"Ugonjwa huu nimeishi nao kwa miaka 20, nimeteseka sana ndani ya ndoa nimemwagiwa maji ya moto na mume wangu, nimeachiwa alama ya maisha", amesema Rehema.

Kwa upande wake Rais wa chama cha madaktari wa Fistula nchini, Dkt. James Chapa, amesema kuwa ugonjwa huo unawaathiri wakina mama kiuchumi, kijamii na kisaikolojia.

Hayo yanajiri wakati Dunia ikijiandaa kuadhimisha siku ya kutokomeza fistula ambayo huadhimishwa Mei 23, aidha maadhimisho ya kutokomeza fistula duniani kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo Fistula ni ukiukwaji wa haki za binadamu-tuitokomeze sasa.