Jumatatu , 18th Jan , 2021

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic, amesema kuwa ameyapokea maagizo ya Rais Magufuli, na kwamba walikwishaanza kuchukua hatua za ujenzi wa shule ya msingi King'ong'o ikiwemo kutenga milioni 80, baada ya wao kuona video ikionesha changamoto ya shule hiyo.

Beatrice Dominic, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 18, 2021, wakati akizungumza kwenye kipindi cha DriveShow cha East Africa Radio, yakiwa yamepita masaa kadhaa tu tangu Rais Dkt. Magufuli, alipotoa maagizo ya kwamba akija Dar es Salaam, akute ujenzi wa shule hiyo umekamilika na wanafunzi hawakai chini, huku akishangazwa na viongozi wa mkoa huo wapo lakini hawashughulikii kero hiyo.

"Awali ya yote nimeyapokea maelekezo ya Mh Rais, sisi tangu tulipoona hiyo clip hatukukaa kimya kila mtu alishangaa kwa sababu ni taarifa ambazo hazikuwahi kufika ofisini kwangu na hata kwenye ukaguzi wa kawaida Afisa Elimu alikuwa hajawahi kutuambia, tangu jana mimi na timu tupo site", amesema Beatrice

Aidha ameongeza kuwa, "Na tayari kazi ya kuchimba misingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa imeanza, kikubwa tunachofanya ni kupata fundi ambaye atakamilisha hii kazi kwa muda mfupi unaowezekana na ubora unaotakiwa, lakini tumeshaweka oda kwa ajili ya ununuzi wa madawati".