Baada ya Zitto kuumwa, Madaktari wampa ushauri

Ijumaa , 14th Feb , 2020

Katibu wa Uenezi wa Chama cha ACT Wazalendo Ado Shaibu, amesema kuwa kwa sasa afya ya kiongozi wa chama hicho na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, imeimarika na tayari ameruhusiwa kutoka hospitali na madaktari wake wamemwambia kwa sasa anaweza kusafiri.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Ado Shaibu ameyabainisha hayo leo Februari 14, 2020 wakati EATV&EA Radio Digital, ilipotaka kufahamu hali ya Mbunge huyo, baada ya hivi karibuni kuelezwa amelazwa nchini Marekani.

"Ndugu Zitto anaendelea vizuri hayupo tena Hospitali na tunatarajia Februari 18, atakuwepo mahakamani, ila bado sijajua mpangilio wake wa safari kwamba lini atafika na madaktari wameruhusu kwa hali yake ya sasa anaweza akasafiri" amesema Ado Shaibu.

Taarifa za kuumwa na kulazwa nchini Marekani, zilitolewa Februari 10, 2020 na mdhamini wake Ray Kimbita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam, baada ya tarehe hiyo Mbunge Zitto kutoonekana mahakamani.