Jumanne , 31st Jan , 2023

Christina Dotto mama wa binti wa miaka 11 anayesoma darasa la 4 jijini Mwanza, anaomba msaada wa matibabu kwa binti yake anayedaiwa kubakwa na baba yake mzazi kuanzia mwanzoni mwa 2022 na kusababishiwa maumivu makali ya kiuno, mgongo na kuwa na maumivu kwenye kizazi na anatokwa usaha.

Christina Dotto, Mama wa binti aliyebakwa

Mama huyo amesema mzazi mwenzake huyo ambae haishi nae alimuomba mtoto huyo aende nyumbani kumsalimia ndipo akaanza kumbaka binti yake huyo huku akimtishia, anasema tayari baba huyo ameshahukumiwa kifungo cha maisha jela lakini hali ya binti yake huyo siyo nzuri kutokana na kulalamika kuumwa mara kwa mara.

"Wakaniambia kwani hauna taarifa?, mbona huyo mume wako huwa analala na mwanao? Mke mwenzako ameshashtaki mara nne, basi nikampeleka mtoto hospitali ikagundulika ameshalala nae tena siyo mara moja na mtoto alikuwa amedhoofika na kutoa usaha kizazi kilikuwa kimeshaharibika ninachotaka mimi mwanangu akachunguzwe kizazi kama kinafaa naomba serikali inisaidie mtoto wangu apone," ameomba Mama huyo

Dkt. Esther Kafururu ni dakatari wa hospitali ya wilaya ya Nyamagana anaeleza athari za ubakaji alizopata binti huyo na kushauri aendelee na matibabu.

"Huyu mtoto apate mwendelezo wa matibabu lakini pia hajapata darasa la mambo ya saikolojia maana ameathirika kwa kiwango kikubwa sana lazima apate muendeleo pia wa kutibiwa saikoloji walau akili yake ikae sawa tunaomba Watanzania wamsaidie na apate bima ya matibabu," amesema Daktari huyo