Jumamosi , 31st Mei , 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesifu jitihada za Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mchango wake mkubwa katika kupigania Afya ya Mama na Mtoto.

Rais Kikwete alipokutana na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon Toronto, Canada

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesifu jitihada za Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mchango wake mkubwa katika kupigania Afya ya Mama na Mtoto.

Bw. Ban Ki Moon ametoa pongezi hizo tarehe 30 Mei,2014 wakati alipokuwa akizungumzia juhudi za kumuokoa Mama na Mtoto baada ya Mwaka 2015, mwishoni mwa mkutano wa siku 3 kuhusu Afya ya Mama na Mtoto kama ilivoainishwa katika Malengo ya Milenia .

Rais Kikwete na Waziri Mkuu wa Canada Bw. Stephen Harper, kwa miaka minne wamekuwa Wenyeviti Wenza wa Kamisheni ya Habari na Uwajibikaji katika masuala ya Afya ya Mama na Mtoto , ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vifo vya Watoto wachanga na Mama wajawazito vinapunguzwa kwa nusu ifikapo Mwaka 2015.

"Napenda kumpongeza Rais Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika jitihada hizi za kupunguza vifo vya Watoto na akina Mama. Rais Kikwete na Waziri Harper wamedhihirisha uongozi katika kukuza Afya ya Mama na Mtoto, nawapongeza sana " Bw. Ban Ki Moon amesisitiza na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano wa Canada wa kuchangia zaidi katika jitihada hizi.

Pamoja na mafanikio hayo, Rais Kikwete amesema bado jitihada zinahitajika katika kuhakikisha mafanikio haya yanaimarishwa zaidi na kwamba hayapotei .

“Bado tunahitaji wataalamu wa Afya wenye ujuzi , vifaa na teknolojia ya kisasa" Amesema na kuongeza kuwa bado zinahitajika juhudi za pamoja katika kusimamia mafanikio yaliyokwisha kupatikana.

Bw.Ban Ki Moon pia amesema Afya ya Mama na Mtoto ni ajenda muhimu kupigania hata baada ya Mwaka 2015 kwani ni muhimu kwa maendeleo.

Rais Kikwete pia amehudhuria chakuala cha jioni kilichoandaliwa na wafanya biashara wa Canada na Tanzania ambapo ameelezea umuhimu wa biashara na uwekezaji nchini kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa Tanzania.

Rais amesema Tanzania inahitaji vitega uchumi zaidi kutoka Canada na hivyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Canada kuja kuwekeza Tanzania.

Rais Kikwete anatarajia kuondoka Toronto leo tarehe 31 Mei, kurejea Dar es Salaam, kupitia Marekani.