Ijumaa , 12th Mei , 2023

Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Kamilius Membe, amefariki dunia muda mfupi uliopita katika Hospitali ya Kairuki mkoani Dar es Salaam.

Bernard Membe enzi za uhai wake

Taarifa za awali zinaeleza kuwa alipata changamoto ya kifua na kupelekwa hospitalini hapo na baadaye kufariki, Alfajiri ya leo Mei 12, 2023.

Ifuatayo ni sehemu ya maisha ya Bernard Membe kwenye elimu, familia, siasa na uongozi.

Bernard Kamilius Membe alizaliwa Novemba 9,1953, huko Rondo, Chiponda, katika Mkoa wa Lindi, akiwa ni mtoto wa pili kati wa watoto saba (7) waliozaliwa katika familia ya Mzee Kamillius Anthony Ntachile na Mama Cecilia John Membe.

Bernard Membe ni Mmwera, na kama ilivyo desturi ya Wamwera, watoto hutumia jina la ukoo wa Mama. Hivyo watoto wote saba wa familia hii ya Mzee Kamillius wamekuwa wanatumia jina la upande wa mama yao, Cecilia, yaani Membe.

Chini ni hatua za kupata elimu alizopitia Membee.
1962 – 1968: Elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Chiponda, Lindi.
1969 – 1972: Elimu ya Sekondari, (O-level) Namupa Seminary, Lindi
1973 – 1974: Kidato cha tano na sita (A-level) Itaga Seminary, Tabora
1975 – 1980: Aliajiriwa serikalini (Ofisi Ya Rais).
1981 – 1984: Alipata Shahada ya kwanza katika tasnia ya Sayansi katika maswala ya Siasa na mahusiano ya kimataifa (Bachelor Political Science and International Relations)
1985 – 1989: Aliendelea na ajira yake serikalini katika ofisi ya rais
1990 – 1992: Alipata Stashada ya Uchumi, Mahusiano ya Kimataifa na Sheria za Kimataifa (Masters- Economics, International Relations and International Law)
1993 – 1994: Alirudi serikalini kuendelea na kazi kama mchambuzi wa mambo ya ulinzi na usalama

Bernard Membe ni miongoni mwa waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Oljoro, Arusha, kati ya mwaka 1975 na 1976.
Mwaka 1978, Ndugu Membe alipata Mafunzo ya sheria za Jinai na usalama wa nchi, nchini Uingereza. Aidha, mwaka 1980, Ndugu Membe alipata mafunzo ya siasa, katika Chuo cha Chama cha Mapinduzi (CCM), Kivukoni, Dar es Salaam.

Kwenye maisha ya familia Ndugu Bernard Membe alifunga ndoa Takatifu mwaka 1986 na Dorcas Richard Masanche, katika Parokia ya Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam. Ndugu Membe na mama Dorcas wamejaliwa kupata watoto watatu, Cecilia, Richard na Denis.

Maisha ya uongozi ya Bernard Membee yalianza katika hatua mbalimbali lakini mwaka 2000, aliingia Bungeni baada ya kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Mtama, kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka 2005, Bernard Membe alichaguliwa tena na wananchi wa Jimbo la Mtama kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Tofauti na kipindi cha nyuma, Bernard Membe alianza muhula wa pili wa Ubunge, Januari 2006, kama ‘front bencher’ baada ya kuteuliwa na rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.

Kufuatia mabadiliko ya baraza la Mawaziri mnamo mwezi Oktoba, 2006, Bernard Membe alihamishwa Wizara na kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini.

Hata hivyo miezi michache baadae, yaani Januari 2007, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alimteua Bernard Membe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa baada ya aliyekuwa anashikilia wadhifa huo - Dr. Asha Rose Migiro kuteuliwa na Katibu Mkuu Baraza la Umoja wa Kimataifa na kuwa Naibu Katibu mkuu wa baraza hilo.

Bernard Membe amehudu katika nafasi hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tangu 2007 hadi 2015, akiwa ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo kwa miaka mingi mfululizo, akitanguliwa na Rais Kikwete ambaye alidumu katika Wizara hiyo kwa miaka 10 mfululizo.