Jumanne , 3rd Mei , 2016

Bunge limeombwa kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dokta John Pombe Magufuli, za kuongeza ukusanyaji wa kodi utakaochangia upatikanaji wa fedha za kuendeleza miradi ya maendeleo nchini.

Ashatu Kijaji

Maombi hayo yametolewa Bungeni Mjini Dodoma, Mei 2, 2016 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Ashatu Kijaji, wakati akijibu maswali ya wabunge, kwaniaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Philip Mpango.

Dokta Kijaji alisema kuwa kuongezeka kwa mapato ya serikali ndiyo njia pekee ya kuondokana na nakisi ya bajeti inayochangia kukwama kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo nchini.

Aidha, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Ashatu Kijaji, aliliambia Bunge kuwa serikali itaendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kupanua wigo wa kodi, kila anayestahili kulipa kodi kulipa kodi stahiki na kuweka mazingira rafiki au wezeshi kwa mlipa kodi.

"Hatua hii inalenga kuongeza mapato ya serikali, kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje inayoambatana na masharti kadhaa mabayo baadhi yake yanaleta usumbufu na hasara kwa taifa". Alisisitiza Dokta Kijaji.

Aliahidi kuwa serikali itaendelea kutuma fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ukiwemo mradi wa maji wa Fumagila, ulioko katika Jimbo la Nyamagana, mkoani Mwanza.

Dokta Kijaji alikuwa akijibu swali la nyongeza, lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Stanslaus Mabula, aliyetaka kujua serikali itapeleka lini fedha, kiasi cha shilingi 200m kwaajili ya kukamilisha mradi huo unaotarajiwa kuwanufaisha watu 16,000, uliochukua muda mrefu kukamilika.