Alhamisi , 29th Mei , 2025

Mahakama ya wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa imemhukumu Theonas Mwinuka maarufu kama Razack, mkazi wa Ruaha Mbuyuni, kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumjeruhi mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 8, kisha kumtupa mtoni.

Theonas Mwinuka maarufu kama Razack

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Tumaini Maleko, kufuatia ushahidi thabiti uliowasilishwa na upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili wa serikali Majid Matitu na Kashindye Maganga.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mwinuka alitenda kosa hilo la kikatili katika kijiji cha Ruaha Mbuyuni, ambapo alitumia nguvu na kusababisha majeraha makubwa kwa mtoto huyo kabla ya kumtupa mtoni kwa lengo la kuficha ushahidi.

Hakimu Maleko alieleza kuwa mahakama imezingatia ushahidi wa muhanga, mlezi wake, daktari na maelezo ya mshtakiwa, na kuthibitisha kosa hilo pasipo shaka yoyote.

Mwinuka amehukumiwa chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya mwaka 2022), Kifungu cha 130(1)(2) pamoja na Kifungu cha 131(3), vinavyohusiana na makosa ya ubakaji kwa watoto.

Mahakama imesisitiza kuwa hukumu hiyo iwe fundisho kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kikatili dhidi ya watoto, ikieleza kuwa haki za mtoto ni za msingi na zinapaswa kulindwa kwa nguvu zote za kisheria.