Jumanne , 23rd Sep , 2025

"ICC imejidhihirisha kuwa haina uwezo wa kushughulikia na kushtaki uhalifu wa kivita uliothibitishwa, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa mauaji ya halaiki, na uhalifu wa uchokozi"

Nchi Wanachama watatu wa Muungano wa Nchi za Sahel katika Afrika Magharibi zimetoa taarifa ya pamoja zikiishutumu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC na kueleza mipango yao ya kujiondoa katika mahakama hiyo  na badala yake kutengeneza utaratibu wa kiasili wa uimarishaji wa amani na haki ndani ya mataifa hayo.

Mataifa hayo ya Afrika Magharibi yanayoongozwa  kijeshi ya Burkina Faso, Mali na Niger yametangaza jana Jumatatu Septemba 22 kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, yakiitaja kuwa ni chombo cha kibeberu cha ukoloni mamboleo.

Tawala hizo za kijeshi zilizotwaa mamlaka za Bamako, Ouagadougou na Niamey baada ya mapinduzi kati ya 2020 na 2023 zimeungana katika shirikisho linaloitwa Muungano wa Nchi za Sahel (AES) na kujitenga na muungano wa Afrika Magharibi, ECOWAS haswa kutoka kwa mtawala wa zamani wa kikoloni Ufaransa.

Mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague, imetajwa na mataifa hayo kama chombo cha ukandamizaji wa ukoloni mamboleo ulioko mikononi mwa ubeberu "ICC imejidhihirisha kuwa haina uwezo wa kushughulikia na kushtaki uhalifu wa kivita uliothibitishwa, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa mauaji ya halaiki, na uhalifu wa uchokozi," walisema.

Burkina Faso, Mali na Niger zimeegemea zaidi nchini Urusi, ambayo Rais Vladimir Putin amekuwa chini ya hati ya kukamatwa kwa ICC tangu Machi 2023 kutokana na vita vya Ukraine. Nchi hizo za Afrika Magharibi zinakabiliwa na ghasia mbaya kutoka kwa makundi ya kijihadi yanayohusishwa na Al-Qaeda na Islamic State, licha ya majeshi yao pia kushutumiwa kwa uhalifu dhidi ya raia.

ICC ilianzishwa mwaka 2002, dhamira ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ni kuwashtaki wahusika wa uhalifu mkubwa zaidi, kama vile uhalifu wa kivita, pale nchi wanachama zinapokosa nia au uwezo wa kufanya hivyo zenyewe.