Jumanne , 4th Aug , 2015

Chama Cha Mapinduzi (CCM), MKoa wa Arusha kimesema viongozi ambao wameweka mguu mmoja CCM na mwingine upinzani, ni bora watoke mara moja wawaachie chama chao kuliko kuhujumu chama hicho, vinginevyo watashughulikiwa vikali.

Katibu wa ccm wilaya ya Arusha mjini Feruzi L. Bano kulia akimpa maelekezo mtia nia wa kugombea ubunge wa jimbo la Arusha mjini kwa tiketi ccm

Akizungumza leo Jijini Arusha, kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Arusha Mjini, Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Feruzy Bano amesema katika uchaguzi wa kura za maoni wamegundua hujuma zilizofanywa na viongozi wa CCM, jambo ambalo ni shida.

Ametoa mfano wa hujuma waliofanya ni kuwatisha wanachama na hasa maeneo ya umasaini, na kusababisha wapiga kura kujitokeza wachache 7,251 kati ya 27,000 wanachama hai.

Amesema ni bora wakatoka wamfuate wanayemtaka ,kuliko kubaki katika CCM wakati kimwili na roho hawako huko na wapo katika uchunguzi kisha watashughulikiwa.

Aidha ameonya wagombea nafasi ya Udiwani waoshinda nafasi zao, ambao wana mpango wa kujitoa baadaye ili kuipa ushindi Chadema, waache kufanya hivyo maana cha moto watakiona.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Godfrey Mwalusamba, amesema kuwa wanaoeneza uzushi kuwa CCM Arusha ina hali mbaya, wananchi wawapuuze na kudai ipo imara na viongozi wanaohujumu chama wanajulikana na watashughulikiwa baada ya uchunguzi wao kukamilika.

Amesema CCM haitaki kubaki na watu ambao wamebeba maono ya watu au mtu fulani, hivyo bora wakamfuata alikokwenda baba yao aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa.

Mbunge Viti Maalum, Catherine Magige amesema ni vema viongozi wote wanotaka kutoka kwa kuendekeza makundi ndani ya chama hicho, bora wakatoka mara moja wawaachie chama chao, kwani makundi yaliishia Dodoma na sasa timu moja ya kumnadi Dk. John Magufuli.