Jumanne , 6th Oct , 2015

Vyama vikuu vyenye upinzani nchini Tanzania katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu vimeendelea kuchuana katika kampeni kanda ya kaskazini huku CCM wakizindua kampeni ya 'Elimu ya Mpiga Kura' kwenye majukwaa.

Wagombea Nafasi ya Urais Mh. Edward Ngoyai Lowassa na Mh. John Pombe Magufuli.

Katika mikutano ya hadhara katika Wilaya ya Karatu Mkuu wa Msafara wa kampeni ya Chama hicho Alhaji Abdallah Bulembo ametumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananci jinsi ya kupiga kura hiyo.

Kwa upande wake mgombea urais kupitia chama hicho Mh. John Pombe Magufuli amewataka madiwani watakaochaguliwa kupitia chama hicho kusimamia halmashauri katika kufuta ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo ili kuinua uchumi wa wafanyabiashara hao.

Wakati huo huo mgombea urais wa UKAWA kupita CHADEMA, Mh. Edward Lowassa akiwa katika jimbo lake alilohudumu kwa miaka 20 akiwa na CCM jimbo la Monduli amesema hatowabeba wagombea wa CCM kwa kuwa alikuwa mbunge kupitia chama hicho lakini kwa sasa ataendelea kuwanadi wagombea wa umoja huo.

Aidha Mh Lowassa amesema ataendelea kuwatumikia wakazi wa jimbo hilo kama alivyokuwa mbunge na kuhakikisha malalamiko yao yote yanapatiwa ufumbuzi ikiwemo wananchi wa jimbo hilo kufaidika na rasilimali zilizopo.