Jumatano , 7th Jan , 2015

KAMATI ya siasa ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini mkoani humo, kimelaani kitendo cha jumuiya ya umoja wa vijana wa chama hicho, kufanya maandamano na kufunga ofisi za CCM, wilaya hiyo.

Wanachama wa Chama Cha Mapundizi wakiwa katika moja ya Mikutano ya kukiimarisha Chama.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini kanali Mstaafu Tajiri Maulidi ametoa kauli hiyo wakati akitoa tamko la chama, baada ya kamati ya siasa ya halmshauri kuu ya (CCM) wilaya hiyo, kukaa na kujadili tukio ambalo limefanywa na (UVCCM) ni la kukidhalilisha Chama.

Amesema vijana hao hawakutakiwa kufanya fujo mbele ya ofisi za CCM, huku wakifunga ofisi, bali walitakiwa kuandika barua za malalamiko yao juu ya viongozi ambao hawana imani nao, ili ijadiliwe na kamati ya siasa, na kama kuna ukweli viongozi hao wachukuliwe hatua, na siyo kukichafua chama.

Tamko hilo limekuja siku moja baada ya baadhi ya vijana wa (UVCCM) kufunga ofisi za (CCM) wilaya, wakishinikiza katibu wa wilaya Charles Sangula, katibu wa siasa na uenezi wa wilaya Charles Shigino, na mchumi wa wilaya hiyo Ahmed Mapalala waondolewe katika chama.

Vijana hao wamedai hawataki kuongozwa na viongozi hao kwa kuwa ni wasaliti wamekuwa wakikiuza chama na kuwapa nafasi wapinzani, huku wakiwatolea kauli za matusi na kuudharau umoja huo wa vijana, hali ambayo wanahofia kukosa viti vingi vya uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo, amesema kamati hiyo ya Siasa, bado inaendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio la vijana hao la kumshambulia kwa kipigo diwani wa Kata ya Ndala, katika manispaa ya Shinyanga George Sungura kupitia CHADEMA aliyepigwa akiwa anapita katika eneo la ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga Mjini