Jumatano , 2nd Jan , 2019

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt Bashiru Ally, amesema chama hicho hakitasita kuyakata majina ya wananchama wake ambao watabainika kutumia njia ambazo si halali ili kuhakikisha wanapewa nafasi ya kugombea uongozi kwenye chama hicho.

Kamati Kuu Chama Cha Mapinduzi

Dkt Bashiru ametoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Bukoba, ambapo alikutana na viongozi mbalimbali wa CCM, pamoja na viongozi wa vyama vya mazao.

"Ukifuatilia siasa za CCM wakati wa uchaguzi, ilikuwa ni za kutumia pesa, kununulia wanachama kadi, mfumo wa uteuzi umebadilika, kura za maoni watu wengi hawatuhusika, si kwa sababu hawatakiwi kupata haki bali kutakuwa na mchujo utaosimamiwa vizuri," amesema Dk Bashiru.

Aidha kuelekeea Uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu, kiongozi huyo amewataka wananchi kutowachagua viongozi wanaowapa hela, kwakuwa uchaguzi wa serikali za mitaa ni uchaguzi muhimu kuliko uchaguzi mkuu kwa sababu serikali za mitaa ndizo zilizo karibu na wananchi na zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.

"Tumeanza kuhamasisha wanachama wenye sifa waanze kujitokeza hasa sehemu za vitongoji na vijiji, kwasababu uchaguzi wa mwaka huu utakua ni uchaguzi wa wanachama wenye sifa, sio wanachama wanaoweza kufanya siasa za kutumia pesa au kupendeleana," ameongeza Dkt Bashiru.