
Akizungumza Jumatatu katika Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), mkoani Dar es Salaam, Khatibu amempongeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa hatua ya kuwaleta pamoja viongozi wa kitaifa na watendaji wa vyama kwa lengo la kutoa elimu na kuimarisha msingi wa demokrasia.
“Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tunakupongeza sana kwa kazi nzuri ya ulezi wa vyama vya siasa. Umeona umuhimu wa kutukutanisha hapa ili kupitia Sheria ya Gharama za Uchaguzi, jambo hili ni jema kwa sababu linapunguza kasoro katika uchaguzi wetu,” amesema Khatibu.
Amesisitiza kuwa historia inaonesha baadhi ya vyama na wagombea walikuwa na uelewa mdogo walipotakiwa kuwasilisha taarifa za gharama za uchaguzi, jambo lililosababisha kuibuka kwa kasoro kubwa.
“Sheria hii ilipokuja mwaka 2010, watu wengi hawakuwa na uelewa. Wengine walijaza gharama za uchaguzi hewa wakidhani baada ya uchaguzi wangerejeshewa fedha. Watu walitengeneza risiti za kughushi, kumbe haipo hivyo. Hivyo basi leo tunatarajia kupata elimu ya kutosha,” amefafanua.
Khatibu amewataka viongozi na watendaji wa vyama kuchukua kwa umakini mkubwa mafunzo hayo ili, kuelekea Uchaguzi Mkuu, zoezi la kampeni na uchaguzi kwa ujumla liendeshwe kwa uwazi, uadilifu na kuepusha migogoro.