Jumanne , 7th Sep , 2021

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maelekezo matatu kwa serikali kuhusu ununuzi wa mahindi ya wakulima, vituo vya kununulia mahindi pamoja na bei ya mbolea nchini.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, baada ya chama hicho kusikia malalamiko ya wakulima kuhusu uhaba wa masoko ya mahindi, ambapo kimeilekeza serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kununua mahindi katika mikoa yenye uzalishaji mkubwa.

"Baada ya maagizo ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuhusu utafutaji wa masoko ya mahindi, NFRA na Bodi ya Mazao Mchanganyiko ilitenga fedha kununua mahindi, na taarifa zilizopo ununuzi unasuasua kutokakana na fedha kuisha, sasa hatuwezi kukaa namna hii wakulima wetu hawana pa kuuza mahindi yao, hivyo maagizo ya chama kwa serikali, watafute fedha popote wanapojua na suala la kununua mahindi liendelee,” amesema Chongolo.

Aidha, katika Hatua nyingine, baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wakulima kuhusu uchache wa vituo vya ununuzi wa mahindi, chama kimeilekeza serikali kupitia Wizara ya Kilimo, kuongeza vituo vya ununuzi na gharama za usafiri wasibebeshwe wakulima kama inavyofanyika sasa kwa wakulima waliopo pembezoni mwa vituo vya ununuzi.