Jumapili , 28th Mei , 2023

Wananchi wilayani Mufindi mkoani Iringa, wameshauriwa kuendelea kuunga mkono Chama cha Mapinduzi na kuacha kusikiliza porojo za watu wengine kwa sababu mafanikio hayaji siku moja.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Chongolo

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Chongolo, wakati akizungumza katika mikutano mbalimbali ya mashina na wananchi wa mji wa Mafinga na kuwataka kuacha kudanganywa na kutengenezewa matumaini hewa kwa sababu hakuna miujiza kwenye mafanikio kwani kila kitu ni hatua.

"Muache kudanganywa wapo watu wanakuja wanapiga porojo kweli kweli ni mabigwa wa kuwatengenezea watu matumaini hewa hakuna miujiza kila kitu kinaenda kwa hatua watu waliotamani kukimbia kwenye mafanikio wengi wamejikwaa wakapotea kwa sababu mafanikio ni hatua na lazima waambiwe ukweli," amesema Chongolo

Aidha Chongolo ameongeza kuwa, "Na sisi viongozi twende chini tuwaambie wananchi ukweli wasiyumbishwe wakadhani kila jambo linakuja kwa miujiza kumbe ni hatua kwa hatua na utaratibu,unapanga na unatekeleza hakuna jambo linalotoka hewani".

Chongolo yupo ziarani mkoani Iringa, akiambatana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Sofia Mjema na Katibu wa NEC, Oganaizesheni Issa Haji Ussi Gavu.