Jumamosi , 24th Oct , 2020

Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba, amesema atakapopata ridhaa ya kuwaongoza Watanzania, serikali yake itashirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Kimataifa ili kuweza kuwekeza katika mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Profesa Lipumba ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi wa Kijiji cha Kipindimbi, Kata ya Njinjo, jimbo la Kilwa Kaskazini ambapo amesema serikali ya CUF kwa kushirikiana na wananchi itahakikisha wananchi wanaondokana na maafa ya mafuriko.

''Pana tatizo ambalo linaweza kuwa la muda mrefu tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ni tatizo ambalo tayari limeshatufikia, nchi zilizoendelea zimekuwa zikizalisha hii hewa ukaa ambayo imeongeza joto Duniani tunahitaji tuwe na serikali makini yenye huruma itakayoshirikiana na wananchi na Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo la mabadiliko ya tabia nchi", amesema Profesa Lipumba.

Pamoja na hayo Profesa Lipumba amesema kuwa atakapoingia Ikulu ataanza kujenga barabara ya kutoka Nangurukuru - Liwale kwa kiwango cha lami ili kuwafungulia uchumi wakazi wa maeneo hayo na maeneo mengine.