Jumamosi , 12th Jan , 2019

Jumla ya wanafunzi 30 wa shule ya msingi binafsi ya Little Treasure, iliyoko Manispaa ya Shinyanga, wamenusurika kifo baada ya kupata ajali wakirejea nyumbani kuto shule.

Basi la shule lililoanguka

Chanzo cha ajali ni dereva wa basi hilo, Emmanuel Faustine (32), ambaye alikuwa akichati na simu ya mkononi huku akiendesha, Januari 10 majira ya ya saa 9 alasiri katika eneo la Kalogo mjini humo.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, Kamishina Msaidizi (ACP) Simon Haule, amesema wanafunzi 30 walikuwa wamesalia kwenye basi hilo na hakuna aliyepoteza maisha zaidi ya kupata majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva ambaye alikuwa akichati na simu wakati akiendesha hatua ambayo ilisababisha kutumbukia mtaroni na kusababisha ajali na mwenyewe kukimbilia kusikojulikana.

Jeshi la Polisi linamsaka dereva wa basi hili ambaye alikimbia mara baada ya kusababisha ajali, ili achukuliwe hatua kali za kisheria na liwe fundisho kwa madereva wengine ambao wamekuwa wakisababisha ajali za lazima na kugharimu maisha ya watu pamoja na kuwapatia ulemavu”, amesema Haule.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa, Dk. Albert Masigati amesema alipokea wanafunzi 30 na baada ya kuwapatia matibabu, 26 waliruhusiwa na kubakia wanne wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.