Jumamosi , 23rd Aug , 2014

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk.Reginald Mengi amesema viongozi wa nchi wanachama wanapaswa kuhamasisha muamko na hamasa ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wananchi ili kufikia malengo yake pamoja na kudumisha jumuiya.

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk. Reginald Mengi.

Dkt Mengi ametoa kauli hiyo katika mlo wa mchana aliowaandalia Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wa tume ya bunge hilo jana Jijini Dar es Salaam, mara baada ya wabunge hao kutembelea vyombo vya habari vya IPP na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na vyombo hivyo.

Dk. Mengi amesema kuwa hata kuvunjika kwa jumuiya hiyo hapo awali kulitokana na jumuiya hiyo kuwa katika ngazi ya viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa na si kwa wananchi, jambo ambalo amesema lilichangia sana hali hiyo kutokea.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Bi. Margaret Zziwa mbali na kuvipongeza vyombo vya habari vya IPP kwa utendaji wake mahiri, ameelezea kuwa moja ya mikakati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa ndio sehemu kuu ya ushiriki wa jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.