Alhamisi , 23rd Dec , 2021

Machi 17, 2021, ni miongoni mwa siku ambazo haziwezi kusahaulika kwa Watanzania, kwani ni usiku ambao zilitolewa taarifa zilizoacha vinywa wazi, vilio, simanzi na majonzi kwa watu wengi nchini, baada ya kutangazwa kifo cha Rais wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Hayati Dkt. John Pombe Magufuli

Taarifa ya kifo chake ilitolewa na Makamu wa Rais wa wakati huo ambaye kwa sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, nchi ilizizima, kila kitu kilisimama kwa muda, nyimbo zikaimbwa, watu wakaomboleza, vilio vikatawala, mataifa kwa mataifa yakatuma salamu za pole kwa nchi ya Tanzania.

Mwaka 2021, sasa upo ukingoni, kifo cha Dkt. Magufuli, ni miongoni mwa matukio yaliyoacha simanzi kwa Watanzania, ikiwa ni mara ya kwanza Watanzania kuzika Rais aliyefariki akiwa madarakani katika miaka 60 ya Uhuru, Tanzania ikaomboleza, Dar es Salaam ikalia na Mama Janeth Magufuli na serikali, Zanzibar ikaitika, Dodoma ikalia, Mwanza ikaomboleza, Chato nako simanzi ikawajaa, chuma kikilazwa kikilazwa kwenye nyumba yake ya milele.

Safari ya Urais ya Hayati Dkt. Magufuli, ilianza mwaka 2015, Watanzania walipompa ridhaa ya kuwaongoza chini ya chama chake cha CCM, na kutikisa kwa kauli zake mbalimbali, ikiwemo 'Hapa Kazi Tu', 'Utumbuaji Majipu', 'Waliozila Watazitapika', 'Wapinzani Wametuchelewesha', 'Wanyonge' na nyingne nyingi ikiwemo 'Nikifa mtanikumbuka, tena kwa mazuri yangu'.

Safari ya maisha ya Dkt. John Magufuli, ilihitimishwa Machi 26 kijjini kwake Chato, mkoani Geita, mizinga 21 ikapigwa kama ishara ya heshima, kwa aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Hayati Dkt. John Magufuli alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 61, katika hospitali ya Mzena ya jijini Dar es Salaam, kutokana na maradhi ya moyo.