Jumatatu , 8th Sep , 2025

Maelfu ya vijana wa Nepal wamemiminika barabarani katika mji mkuu, Kathmandu, wakitaka serikali kuondoa marufuku iliyowekwa kwa mitandao ya kijamii na kukomesha ufisadi unaozidi kuenea nchini humo.

Mitandao mengi ya kijamii ikiwa ni pamoja na Facebook, YouTube, na  X, imefungwa tangu siku ya Ijumaa wiki iliyopita baada ya serikali kufungia mitandao ya kijamii 26 ambayo haijasajiliwa, hatua iliyowachanganya na kuwakasirisha watumiaji.

Mtandao mwengine ulio maarufu kama Instagram una mamilioni ya watumiaji nchini Nepal wanaoutegemea kwa burudani, habari na biashara.

Waandamanaji hao wa Gen Z walianza maandamano yao kwa wimbo wa taifa kabla ya kuanza kutoa maneno makali dhidi ya serikali wakilalamikia kufungwa kwa mitandao ya kijamii pamoja na ufisadi.